TFS YAUNGANA NA WAZIRI MKUU MUFINDI, ASISITIZA NISHATI SAFI NA UWAJIBIKAJI KWA WATUMISHI

Na Mwandishi Wetu, Iringa | Mei 2, 2026

WAZIRI Mkuu leo Mei 2, 2026 amefanya ziara Wilayani Mufindi, Mkoani Iringa, akikagua shughuli za maendeleo na kusikiliza kero za wananchi katika maeneo ya Igowole na Ifwagi, huku akisisitiza matumizi ya nishati safi ya kupikia na uwajibikaji kwa watumishi wa umma.

Akizungumza na wananchi, Waziri Mkuu alisema ni muhimu kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika kulinda mazingira na kuboresha afya za wananchi.

Alisema matumizi ya nishati safi si tu yanapunguza uharibifu wa misitu bali pia yanasaidia kupunguza athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya nishati chafu majumbani.

Aidha, aliwataka wananchi kushirikiana na serikali katika kulinda na kuendeleza miradi ya maendeleo ili iweze kuleta tija kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisisitiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, akitaka wahakikishe wanatekeleza kwa vitendo maelekezo na ahadi zote zinazotolewa kwa wananchi ili kuondoa malalamiko yasiyo ya lazima.

Katika ziara hiyo, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Kanda ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na Shamba la Miti la Sao Hill walishiriki kikamilifu, wakionesha dhamira ya taasisi hiyo katika kuunga mkono juhudi za serikali za uhifadhi wa misitu na uendelezaji wa matumizi ya nishati safi.



Post a Comment

0 Comments