WAZIRI MKUU AWASILISHA BAJETI YA TRILIONI 12.5 KWA MWAKA 2026/27

 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amewasilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka wa fedha 2026/2027, yenye jumla ya shilingi trilioni 12.5 (12,502,356,160,000)

Akiwasilisha hoja hiyo leo Aprili 1, 2026, Bungeni Jijini Dodoma, Dkt. Nchemba alisema kuwa kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 8.73 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida, huku shilingi trilioni 3.77 zikielekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Dkt. Mwigulu amefafanua kuwa bajeti hiyo inalenga kuimarisha utoaji wa huduma za Umma pamoja na kusukuma mbele agenda ya maendeleo katika taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge.

Kwa upande wa mapato, Waziri Mkuu amelieleza Bunge kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zinatarajia kukusanya jumla ya Shilingi Trilioni 2.34 (2,336,528,152,302.47) ambapo jumla ya makusanyo na maduhuli ya ofisi yake ni Shilingi Trilioni 2.4 (2,411,548,152,302.47) ambazo zinatarajiwa kukusanywa.

Aidha, Dkt. Mwigulu amebainisha kuwa kiasi cha Shilingi Trilioni 12.268 (12,268,472,643,000) kitatumika mahsusi kugharamia shughuli za kawaida na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, hatua inayotarajiwa kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.


 

Post a Comment

0 Comments