Kufuatia
taarifa zinazozunguka mitandaoni kuhusu wanaume Tunduma kudaiwa
kupotezewa nyeti zao kwa imani za kishirikina, Mkuu wa Mkoa wa Songwe,
Jabiri Makame, ametoa onyo kali kwa yeyote anayesambaza uvumi huo na
kwamba atakayekiuka amri hiyo atachukuliwa hatua.
Makame ametoa
onyo hilo wakati akizungumza na wananchi katika eneo la Kilimanjaro,
Halmashauri ya Mji wa Tunduma, akisisitiza kwamba imani za kishirikina
zinachangia kuibuka kwa matukio yanayoweza kusababisha kusimama kwa
shughuli za kiuchumi na maendeleo.
Amebainisha kuwa asilimia
kubwa ya walioarifu kupotezewa nyeti zao walikaguliwa na kupatikana
wazima, hivyo kuendeleza taarifa hizo ni kuchochea taharuki na
kusimamisha maendeleo.
Aidha, amewataka wananchi wa Tunduma
kuacha kueneza imani za kishirikina na badala yake wajikite katika kazi
na shughuli za maendeleo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe,
Augustino Senga, amesema tayari watu 26 wako mikononi mwa polisi
kutokana na matukio ya uchochezi.
Baadhi ya wananchi, akiwemo
Rehema Ngonya, wamedai kwamba matumizi ya dawa za kuongeza nguvu za
kiume, ikiwemo “Vumbi la Congo”, ni moja ya sababu zinazoathiri maumbile
yao, huku vijana wengi wakitumia dawa hizo bila uangalifu. Ziara ya
Mkuu wa Mkoa ililenga pia kutoa taarifa ya hali ya usalama kuelekea
Sikukuu ya Pasaka.
0 Comments