MTOTO AIBIWA,AKUTWA AMETELEKEZWA MAKABURINI

 Na Ally Mandai.

Mtoto mwenye umri wa miaka mitatu na miezi kumi wa jinsia ya kike aliyeripotiwa na mama yake kuwa ameibiwa kwa kubebwa kwenye pikipiki na mtu asiyejulikana katika eneo la Kona ya Bwiru, Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza amepatikana baada ya kuokotwa na Wasamaria wema.

Taarifa ya leo Aprili 21, 2026 iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza imeeleza kuwa mnamo Aprili 18 mama mzazi wa mtoto huyo aitwaye Neema Julius Sesela, mwenye umri wa miaka 19, mama lishe na mkazi wa mtaa wa Nyampala “B”, Kata ya Nyamanoro, Wilaya ya Ilemela aliripoti katika Kituo cha Polisi Kirumba kuibiwa kwa mtoto huyo ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sababu za kisheria.

Tukio hilo lilitokea Aprili 18, 2026 mtaa wa Barabara ya Vumbi, Kona ya Bwiru, Wilaya ya Ilemela wakati mama huyo akiwa katika shughuli zake, aligundua kuwa mtoto ameibiwa na mtu huyo aliyeondoka naye kwa kutumia usafiri wa pikipiki ambayo hata hivyo namba zake za usajili hazijafahamika.

Kwa majibu wa taarifa hiyo uchunguzi wa tukio hilo ulianza mara moja kwa kuwahoji watu mbalimbali wenye ufahamu kuhusu tukio hilo ambapo mkazi mmoja wa eneo hilo aliweza kutoa ‘CCTV footage’ iliyoonesha mtu mmoja wa jinsia ya kiume akitoka katika eneo la tukio akiwa amempakia mtoto huyo kwenye pikipiki, ingawa namba zake za usajili hazikuweza kuonekana vizuri.

Mnamo Aprili 20, 2026 majira ya saa 3:30 usiku taarifa zilipatikana kuwa mtoto huyo alitelekezwa kwenye makaburi ya Nyasaka yaliyopo Wilayani Ilemela kabla ya kuokolewa na Wasamaria wema na kumpeleka kwa mwenyekiti wa mtaa wa Nyamuge, Kata ya Nyasaka ambapo alikutwa na michubuko sehemu za usoni na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Sekou-Toure kwa uchunguzi zaidi.

Jeshi la Polisi lilipata taarifa na kufika kwa ajili ya uchunguzi zaidi ambapo Mtoto huyo Wazazi wa mtoto huyo na baba mzazi aitwaye Mwankunja Edward (30) fundi seremala, wote wakazi wa Gana, mtaa wa Nyampala “B”, Wilaya ya Ilemela, wamemtambua mtoto huyo kuwa ni mtoto wao huku uchunguzi wa afya ya mtoto ukiendelea kufanywa katika Hospitali hiyo.

 TANGAZA NASI BIASHARA YAKO UFIKIE MAMILIONI YA WATEJA PIGA 0654414804.


 

 

Post a Comment

0 Comments