■ Ni utekelezaji wa maagizo ya Mh Rais Samia kurudisha heshima ya Tanzanite
■ Mkutano wa wawekezaji na wafanyabiashara wa madini baina ya Nchi mbili kuandaliwa
■ Wafanyabiashara wa madini ya vito kushiriki maonesho ya bidhaa za madini Qatar mwezi April 2026
Katika utekelezaji wa ahadi ya kurejesha thamani na hadhi ya madini ya vito ya Tanzanite, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mkakati thabiti wa kutangaza madini ya Tanzanite nchini Qatar ili kuongeza wigo wa masoko yake na kuvutia uwekezaji na utalii.
Hayo yamesemwa leo tarehe 25 Februari, 2026 na Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde (Mb)alipotembelea Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar na kufanya mazungumzo na watumishi wa ubalozi.
“Soko la Tanzanite miaka ya hivi karibuni lilionekana kushuka kidogo na ndiyo maana hata bei imeshuka. Mhe. Rais ameskia kilio cha wachimbaji na wafanyabiashara wa Tanzanite na kutuagiza Wizara ya Madini kuhakikisha tunarudisha hadhi ya madini haya duniani kote ili yawe na manufaa kwa Taifa letu.”
“Wizara tunatekeleza kwa vitendo maelekezo hayo ya Mhe. Rais. Tutahakikisha tunaendelea kuyatangaza na kuyafikia masoko mbalimbali duniani na kuwaambia Tanzanite inatoka Tanzania na inapatikana kwa wingi”, alieleza Mhe. Mavunde.
Waziri Mavunde alionesha kwamba mkakati huo wa Serikali ni muhimu na umekuja wakati muafaka kwani tumeona baadhi ya Nchi duniani hawafahamu kama madini ya Tanzanite yanatoka Tanzania, hali ambayo inapelekea kutuondolea soko ambalo lingesaidia pia kutangaza utalii nchini.
Vilevile, Mhe. Mavunde alibainisha kuwa Tanzania imebarikiwa madini ya aina mbalimbali yakowemo ya vito, lakini Tanzanite ni ya kipekee na ni utambulisho wa Taifa letu kwani madini hayo hayapatikani popote duniani zaidi ya Tanzania, ni lazima tujivunie huku tukiyatangaza na kulinda sifa hiyo ya kipekee tuliyojaaliwa kuwa na madini hayo.
.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)
0 Comments