RAIS MWINYI ASEMA DHAMIRA YA SERIKALI KILA MWANANCHI ANAPATIWA HUDUMA BORA YA AFYA

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila Mwananchi anapata huduma bora katika kila nyanja ya Sekta ya Afya.


Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 27 Oktoba 2025, baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la huduma za akina mama na watoto katika Hospitali ya Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja.


Amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa hospitali za Wilaya na Mikoa, pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja na Hospitali ya Saratani iliyopo Binguni, ili kufanikisha lengo la kuwa na huduma za uhakika za afya kwa wananchi wote.


Aidha, ameeleza kuwa kukamilika kwa kituo hicho kutabadilisha hali ya huduma za afya katika Mkoa wa Kusini, ambazo hapo awali hazikuwa za kuridhisha, na kwa kiasi kikubwa kutapunguza changamoto zinazowakabili akina mama wajawazito wakati wa kujifungua.

Rais Dkt. Mwinyi amewashukuru wafadhili wa ujenzi huo, wakiwemo Taasisi ya Fumba Port, Lady Fatuma Foundation, na Jaffer Foundation, kwa moyo wao wa ubinadamu na uamuzi wa kutenga fedha kusaidia ujenzi huo.


Amefahamisha kuwa Serikali haiwezi kufanya mambo yote peke yake, hivyo kujitokeza kwa wafadhili na wadau kushirikiana na Serikali ni jambo jema katika kunusuru maisha ya akina mama wajawazito na watoto, pamoja na kukabiliana na changamoto za uzazi.


Rais Dkt. Mwinyi amemuagiza mkandarasi wa ujenzi huo kuhakikisha utekelezaji unafanyika kwa kuzingatia viwango vya ubora na kufupisha muda wa ujenzi kutoka mwaka mmoja hadi miezi tisa kutokana na umuhimu wake kwa jamii.


Akitoa taarifa ya kitaalamu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Mngereza Miraji Mzee, amesema ujenzi huo unaotekelezwa na Kampuni ya Quality Building Constructor, utagharimu shilingi bilioni 2.5 na ni hatua muhimu katika kuimarisha huduma za afya, hususan kwa akina mama wajawazito na watoto.

Aidha, ameeleza kuwa takriban wananchi 9,821 kutoka shehia 21 za Wilaya ya Kusini watahudumiwa katika kituo hicho kwa huduma za uzazi salama, huduma za ultra sound, huduma za watoto wachanga, na maabara.

 


Post a Comment

Previous Post Next Post

Contact Form