WALIVAA KAMA MADAKTARI, KISHA WAKATOWEKA NA MTOTO WA SIKU MOJA

 Mtoto mchanga mwenye umri wa siku moja ameibwa katika Kituo cha Afya Dareda Kati, wilayani Babati mkoani Manyara, baada ya watu wawili wanaodaiwa kujifanya madaktari kuingia katika kituo hicho na kutokomea na mtoto huyo kusikojulikana.

TANGAZA BIASHARA YAKO KWA SHILINGI ELFU 5 UWAFIKIE MAMILIONI YA WATEJA,PIGA 0654414804.

Tukio hilo limezua taharuki kubwa kwa wananchi pamoja na wazazi wa mtoto huyo, ambao kwa sasa wanaendelea na juhudi za kumtafuta mtoto wao, huku mamlaka za usalama zikifanya uchunguzi kubaini watu wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Dareda Kati, Barnabas Qrasani, amesema uongozi wa eneo hilo umepokea taarifa kuhusu tukio hilo na unaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kufuatilia na kubaini kilichotokea.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Madama Hosea Mkanga, amesema uongozi wa Halmashauri unafuatilia kwa karibu tukio hilo na kwamba hatua stahiki zinaendelea kuchukuliwa kwa lengo la kuhakikisha mtoto huyo anapatikana.

Naye Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Babati, Remidius Mwema, amesema mamlaka za usalama zinaendelea na uchunguzi ili kuwabaini na kuwakamata watu wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo, pamoja na kuhakikisha mtoto huyo anapatikana na kurejeshwa kwa wazazi wake.

Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea, huku wananchi wakisubiri taarifa zaidi kutoka kwa mamlaka kuhusu hatua zinazochukuliwa na maendeleo ya jitihada za kumtafuta mtoto huyo.

Post a Comment

0 Comments