Na Moshi saidi
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Crispin Chalamila amesema taasisi hiyo itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kijamii sambamba na mapambano dhidi ya rushwa, akibainisha kuwa msaada walioutoa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali kuboresha huduma za afya, hususan kwa watoto wachanga.
Amesema TAKUKURU ina majukumu makuu mawili ya kuzuia na kupambana na rushwa kupitia elimu kwa umma, tafiti na uchambuzi wa mifumo, huku akimpongeza Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa za kuboresha sekta ya afya, zikiwemo hatua zilizochangia kutambuliwa kwake barani Afrika kama kinara wa huduma za afya ya mama na mtoto. Aidha, alieleza kuwa vifo vya watoto wachanga, hususan wanaozaliwa kabla ya muda, bado ni changamoto inayohitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali, akisisitiza kuwa taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na sekta ya afya kupunguza tatizo hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, ameishukuru TAKUKURU kwa msaada huo akisema unakuja wakati muafaka ambapo mahitaji ya huduma za watoto wachanga ni makubwa na gharama zake ni za juu.
Amesema hospitali hiyo haiwezi kumudu peke yake kukabiliana na mzigo wa wagonjwa wanaohitaji huduma maalum, hivyo msaada huo ni muhimu katika kuokoa maisha ya watoto.
Aidha, amepongeza ushirikiano uliopo kati ya TAKUKURU na ofisi ya wilaya, akibainisha kuwa taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele si tu katika mapambano dhidi ya rushwa bali pia kusaidia jamii, huku akisisitiza kuwa imani ya wananchi kwa TAKUKURU imeongezeka kutokana na utendaji wake mzuri.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Idara ya Watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Daktari Bingwa wa Watoto, Dkt Irene Karamaga, amesema hospitali hiyo inakabiliwa na ongezeko kubwa la watoto wanaozaliwa kabla ya muda, hali inayoongeza uhitaji wa huduma maalum ikiwemo msaada wa vifaa vya kupumulia.
Amesema kwa takwimu za hivi karibuni, karibu mtoto mmoja kati ya wawili anayelazwa katika hospitali hiyo ni njiti, huku idadi ya watoto waliozaliwa kabla ya muda ikifikia zaidi ya asilimia 40 ya wagonjwa wote wa watoto wachanga.
Ameongeza kuwa licha ya jitihada za wataalamu wa afya, bado changamoto ya uhaba wa vifaa na wataalamu bingwa inaathiri utoaji wa huduma na kuongeza hatari ya vifo, hivyo msaada unaotolewa na wadau kama TAKUKURU ni muhimu katika kuboresha huduma na kuokoa maisha ya watoto hao.
.jpeg)
.jpeg)


0 Comments