Maelfu ya
wajane kutoka Wilaya mbalimbali Mkoani Iringa wameungana katika kilele
cha Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani ikiwa lengo ni kutambua
mchango wa Wajane katika jamii pamoja na kuangazia changamoto
zinazowakabili.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mwongozo mpya
wa uratibu wa wajane ambapo Kilele cha Maadhimisho hayo yamefanyika
Mkoani Iringa, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi
maalumu Dkt.Dorothy Gwajima amesema serikali imeahidi kuongeza jitihada
za kuwalinda na kuwawezesha kiuchumi kundi hilo la Wajane kwa kuwapa
huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za afya, ushauri wa kisheria
pamoja na msaada wa chakula na mavazi kwa kushirikiana na mashirika ya
kiraia.
Nae mkuu wa wilaya ya kilolo Rebeka Sanga akimuwakilisha
mkuu wa Mkoa wa iringa,amesema Maadhimisho hayo yanalenga kutambua
mchango wa Wajane duniani na kuwapa haki sawa pamoja na kuhamasisha
jamii kutambua na kuheshimu haki za wajane hasa katika masuala ya
urithi, ajira, na ustawi wa familia zao.
Nae mmoja wa wajane
mkoani Iringa ameishauri jamii kuhakikisha wanaandika wosia ili kuondoa
migogoro kwa familia pindi wazazi wanapofariki.
Siku ya Wajane
Duniani huadhimishwa kila ifikapo Juni 23, kila mwaka ikiwa ni fursa ya
kuangazia hali ya kundi hilo ambalo mara nyingi husahaulika katika
mipango ya maendeleo, licha ya mchango wao mkubwa katika jamii.
0 Comments