DKT. MWIGULU AZURU KABURI LA MWALIMU NYERERE, BUTIAMA

 

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Ijumaa Julai 3, 2026, ametembelea Kaburi la Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, lililopo Butiama mkoani Mara, ambapo ameweka shada la maua kama ishara ya heshima na kumbukumbu kwa mchango mkubwa wa kiongozi huyo katika harakati za ukombozi, ujenzi wa taifa na maendeleo ya Tanzania.

Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya ratiba ya Waziri Mkuu akiwa mkoani Mara kwa ziara ya kikazi inayolenga kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kujionea hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali kwa manufaa ya wananchi.

Mbali na kukagua miradi hiyo, Dkt. Mwigulu anatarajiwa kukutana na wananchi pamoja na viongozi wa serikali na wadau mbalimbali, kusikiliza changamoto zinazowakabili na kutoa maelekezo ya kuzitatua ili kuboresha utoaji wa huduma na kuharakisha maendeleo katika mkoa huo.

Ziara hiyo inaakisi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi, inakamilika kwa wakati na inatoa huduma bora kwa wananchi, sambamba na kuendeleza misingi ya uongozi, uzalendo na uwajibikaji iliyoasisiwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.


 

Post a Comment

0 Comments